61 Watetea Mapendekezo yao Katika Dirisha la Tatu la Shindano la DLIIC

61 Watetea Mapendekezo yao Katika Dirisha la Tatu la Shindano la DLIIC

Shindano la Ubunifu kwa kutumia takwimu la Data for Local Impact Innovation Challenge (DLIIC) linapenda kuwapongeza washiriki 61 (mashirika 12 na watu binafsi 49) waliofikia katika hatua ya kutetea mapendekezo yao katika Dirisha la Tatu la shindano la DLIIC, ambalo lilijikita zaidi katika masuala ya Ajira kwa Vijana na Uwezeshaji wa Kiuchumi.

Dirisha la tatu la shindano la DLIIC lilizinduliwa Desemba tarehe 1 2017 na kufungwa Januari 30 2018. Shindano hili lilitazamia katika maendeleo endelevu lengo la namba 8, ambalo linalenga ukuaji wa uchumi wa pamoja na endelevu, ajira kamili na ya uzalishaji, na kazi nzuri kwa wote. Lengo likiwa kuhakikisha uwezeshaji wa kiuchumi na fursa, hasusani kwa vijana, ni kipaumbele kikubwa kwa Tanzania. Uwezeshaji wa kiuchumi huchangia malengo mengine ya maendeleo, kama vile afya bora (ikiwa ni pamoja na kumaliza ugonjwa wa UKIMWI), usawa wa kijinsia, na kuondoa umasikini na njaa. Mada kuu elekezi katika shindano zilikuwa;

  1. Kuimarisha usawa kati ya mahitaji ya waajiri na ujuzi wa vijana; na kuwaandaa vijana kwa ajili ya soko la ajira,
  2. Kukuza uwezeshaji wa kiuchumi wa vijana, na
  3. Kuendeleza na kuhamasisha uhusiano kati ya vijana na fursa za kiuchumi.

Dirisha la tatu la shindano hili ilikuwa fursa kwa wajasiriamali wa ndani kuzalisha ubunifu mpya, teknolojia, na taratibu za kutumia data kushughulikia masuala ya kiuchumi na ajira yanayowakabili vijana wa kitanzania. Waombaji zaidi ya 365 waliwasilisha mawazo ya jinsi ya kuongeza uajiri wa vijana na uwezeshaji wa kiuchumi. Baada ya mapitio na tathmini kamili, jopo letu la majaji wataalamu walichagua maombi 68 ili kufikia hatua ya mwisho ya shindano – ya kutetea mapendekezo yao mbele ya jopo la majaji  na watazamaji. Tukio hili lilifanyika tarehe 28-29 Machi katika ofisi za dLab jijini Dar es Salaam, na washiriki 61 waliongea.

Akihitimisha zoezi hilo, Bw. Agapiti Manday, Meneja wa Mradi wa DLIIC, alisema DLIIC inafurahi juu ya kuongezeka kwa idadi ya waombaji katika Shindano la Tatu ikilinganishwa na mashindano yaliyopita. “Katika shindano hili tulipokea maombi zaidi ya 365. Namba ya maombi imeenda juu ikilinganishwa na mashindano yaliopita. Ningependa kuwashukuru wote waliofikia hatua hii kwa sababu wakati huu ushindani wa shindano la DLIIC  ulikuwa mgumu sana. Kila mtu alikuwa majiandaa kikamirifu,” alisema Bw Manday.

“Baada ya kuchaguliwa, ni jambo la maana sana kwangu,” alisema Bw Daniel Kapinga mmoja ya washiriki wa dirisha la tatu wa shindano la DLIIC.  Aliongezea kuwa, “Ni fursa kwa Kilimo Forum. Tunaendelea kutumia takwimu kwa kiasi kikubwa ya Big Data katika kilimo kwa ajili ya Tanzania, ambayo itakuwa ni chanzo muhimu cha kwa ajili ya soko la mazao ya kilimo kwa wakulima kufanya maamuzi juu ya zao gani la kuzalisha, mchakato wa kuuza nje. Natumaini kupitia Dirisha la Tatu la shindano la DLIIC, tutafikia lengo hili. Ninafurahi kuwa miongoni mwa washiriki.”

DLIIC tayari imeshatoa ruzuku kwa washindi 22 kutoka kwenye shindano la Kwanza na la Pili. Madirisha haya mawili ya mashindano yalijikita katika lengo la kupunguza mazingira hatarishi ya VVU / UKIMWI na kuboresha huduma za afya kwa jamii nchini Tanzania. Pata maelezo zaidi juu ya jinsi hawa washindi wa awali wanavyotumia takwimu yaani data katika kukabiliana na changamoto za afya kupitia Wasifu wa Mshindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published.