Uzinduzi wa TanzMED, jukwaa la kibunifu la taarifa za afya

Uzinduzi wa TanzMED, jukwaa la kibunifu la taarifa za afya

Ukiwa na swali juu ya afya yako, ni nani utakaye muuliza? Wengi wetu tunawaamini madokta wetu kwa taarifa za kiafya, lakini inakuwaje kama hauwezi kusubiri apointimenti?  Jukwaa jipya linaziweka taarifa hizi muhimu za afya katika ncha ya vidole vya watanzania. Jukwaa hilo, lijulikanalo kama TanzMED, limetengezwa ili kutoa upatikanaji wa taarifa za huduma ya afya na elimu ambazo zimeandaliwa maalum kwa watanzania.

TanzMED kwa sasa inapatikana katika mfumo wa tovuti na programu ya simu ya mkononi. Programu ya TanzMED kwa sasa inapatikana katika Android kupitia Google Play Store. Wakati huo huo tovuti ikiwa inatoa taarifa zile zile kama programu ya simu na kupatikana kupitia www.tanzmed.co.tz

Akizungumza wakati wa uzinduzi jijini Dar es Salaam, mwanzilishi wa TanzMED, Bw. Mkata Nyoni alisema,”Dhumuni kubwa la TanzMED ni  kuhakikisha kuwa jamii yetu inafaidika na ukuaji wa mawasiliano kupitia intaneti, kwa sababu sasa wanauwezo wa kupokea  taarifa za afya popote walipo.” Pia aliongeza, “Tumeamua kuzindua jukwaa hili ili kuhakikisha kuwa jamii zetu zinakuwa na upana mkubwa wa uelewa kwenye masuala ya afya kwa kuwapatia taarifa zenye ubora na zipatikanazo kwa urahisi.”

TanzMED inaiwezesha jamii kusoma makala zilizoandikwa na madaktari waliobobea. Makala zikipatikana kwa namna zote mbili, ukiwa mtandaoni na usipokuwa mtandaoni pale unapozipakua kupitia programu ya simu. Jukwaa hili pia linawapa watumiaji orodha ya vituo vya afya vya karibu. Orodha hii inajumuisha huduma zitolewazo na vituo hivyo lakini pia taarifa kama vituo hivyo vinakubali huduma ya bima ya afya.

TanzMED pia inatoa huduma nyinginezo. Kwa mfano, jukwaa linawawezesha wanawake na wasichana kufuatilia siku zao za hedhi na kuweza kuwatumia ujumbe kupitia simu zao wakiwa wanakaribia siku zao za hedhi. Kumbukumbu hizi zitolewazo kwa wakati zinawasaidia wanawake na wasichana kukabiliana na siku zao vizuri zaidi.

Akielezea zaidi juu ya mafanikio ya TanzMED, Bw, Nyoni alibainisha kuwa zaidi ya watu 700 utembelea jukwaa hili kila siku. Alibainisha kuwa wanaotembelea wengi wapo katika kundi la miaka 25-34, wakifuatiwa na kundi la miaka 18-24. Wanawake wanachukua asilimia 46 ya watu wote wanaoitembelea TanzMED. Hizi takwimu zinaonyesha kuwa upatikanaji wa taarifa za afya ni muhimu kwa wote mwanaume na mwanamke katika kufanya maamuzi juu ya afya zao wenyewe.

“Tusingeweza kufika hapa tulipofika bila kupata msaada kutoka Data for Local Impact Innovation Challenge (DLIIC), bila ya kuwasahau MCC na PEPFAR kwa kutupatia ruzuku na kuweza kuutekelea mradi wetu,”  alibainisha Bw. Nyoni. Aliongeza, “DLIIC haikupatii tu ruzuku, lakini pia wanahakikisha kuwa unakuwa na uwezo wa kitaalam mzuri ili kutekeleza wazo lako. Pia, wanatoa msaada wa kitaalam kwa kukupatia mshauri atakae kuonyesha njia katika utekelezaji wa mradi wako.”

Unaweza fahamu zaidi juu ya TanzMED kwa kutembelea wasifu wa Bw. Mkata Nyoni hapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published.